KUMBUKUMBU YA MIAKA 13 YA AJALI YA TRENI, DODOMA.

Ulikuwa Msiba mkubwa wa Waadventista wa Sabato Tanzania
Na Conges Mramba,Mwanza
JUMATANO,Juni 24 mwaka huu 2015, itatimia miaka 13 tangu ilipotokea ajali ya Treni,huko Igandu na Msagali Mkoani Dodoma na kuua takriban watu 400, huku zaidi ya 700 wakinusurika.
Kumbukumbu hii inatonesha donda katika myoyo ya Washiriki wa Makanisa ya Waadventista wa Sabato hususan wa Mikoa yote ya Ukanda wa Ziwa,likiwemo kanisa la Kirumba.
Ajali hii ya Kihistoria,mbali na kuua Watanzania wengi,ni Kumbukumbu ya Kihistoria kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato hapa nchini Tanzania,na dunia nzima.
Wakati huo,hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan,alituma rambirambi.
Hata Papa John Paul,Kiongozi wa Kanisa Katoliki,alituma salamu za pole kwa Watanzania.Hukuwa msiba wetu peke yetu.
Zaidi ya wanawake 120 waumini wa Kanisa hili waliteketea katika ajali hiyo ya Alhamisi,Juni 24 mwaka 2002,iliyotokea Asubuhi hiyo eneo hilo kati ya Igandu na Msagali.

Hawa wengi walikuwa akina mama wa mikoa ya Mwanza,Shinyanga,Mara na Kigoma,waliokuwa wakitokea mjini Morogoro.
Juni 18 hadi Juni 22 mwaka huo 2002 kulikuwa na Mkutano wa akina mama Waadventista wa Sabato(Adventist Women Ministry Congress) hapo mjini Morogoro.
Akina mama wa Kanisa hili kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu walikwenda kuhudhuria Mkutano ule.Mkutano ule ulihitimishwa siku ya Sabato,Juni 22. Walikuwa zaidi ya 400.
Ilipofika Jumapili,Juni 23 walikwea treni tayari kurejea nyumbani,baada ya Mkutano ule kumalizika.
Wengi walipanda mabehewa ya Daraja la tatu ambayo yalikuwa na nambari 362211,364P,3635,3620M,3642,3617 na 3680.
Mabehewa hayo yalibeba wanafunzi na akina mama hao wa Ki-Sabato.
Nakumbuka,wakati huo nikifanya kazi katika Gazeti la Msanii Afrika, lililomilikiwa na Kampuni ya Sahara Media Group ambayo sasa inamiliki kituo cha Televisheni cha Star,Kiss FM,Radio Free Afrika na King’amuzi cha Continental, nilitumwa kufuatilia ajali ile katika Makao Makuu ya Jimbo la Kusini mwa Ziwa Nyanza(SNC),Pasiansi.
Nilimkuta Mchungaji  Daudi Makoye(Sasa Mwenyekiti wa Mara Conference),ambaye hakuwa tayari kutoa tamko.Hata wafanyakazi wengine hapo Pasiansi,hawakuwa tayari kusema kitu,wakati Mwenyekiti wa SNC niliambiwa alikuwa kaondoka siku hiyo kwenda Dodoma kutambua maiti.
Mwanamke mmoja,aliniambia kwa masharti ya kutotajwa jina kwamba wanawake takriban 100 wa makanisa ya Mwanza tu waliangamia katika ajali ile ya kutisha.
“Jana Alasiri(Juni 24) tulipata simu kutoka Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma,kwamba kati ya maiti 200 waliokuwepo uwanjani hapo;100 ni Wasabato wa mikoa ya Mwanza,Mara,Shinyanga na Kigoma!”Ofisa huyo wa Jimbo la South Nyanza aliniambia.
Nilikwenda Ofisini(Ilemela)nikaandika habari iliyotoka kwa kichwa cha habari, “Waumini 100 wa  Kanisa la Wasabato wahofiwa kufa!”
Nilifika Kanisa la Mabatini mchana,nikakuta watu wakilia,niliambiwa Kirumba na Pasiansi kulikuwa na kilio kikubwa…Bunda,Musoma,Tarime,Busega na hata vijiji vya Suguti huko Majita Mkoani Mara kulikuwa na majonzi makubwa.Ulikuwa msiba mkubwa,msiba wa kila mtu.
Naam, miaka 13 imepita sasa tangu ajali ile ya kutisha itokee.Wengi wamesahau,ndiyo maana tunawakumbusha hapa.
  
         ILIKUWA AJALI YA KUPANGWA?
Waziri mkuu,Frederick Tluway Sumaye(wakati huo),alisema ajali ile iliyotokea Dodoma na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 250 haikuwa hujuma,bali ajali ya kawaida ya kibinadamu(Tragic accident).
Wakati huo,kulikuwa na mgogoro baina ya wafanyakazi na Menejimenti ya lililokuwa Shirika la Reli(TRC),wakidai mafao yao.
Miaka micache baadaye,nilihudhuria msiba wa mmoja wa wafanyakazi wa SOUTH NYANZA CONFERENCE nikawasikia baadhi ya akina mama walionusurika katika ajali ile wakisema,ilikuwa ajali ya kupangwa.
“Walitusimanga(wafanyakazi wa treni ile),walikuwa wakitwambia tungeona hata kabla ya safari kuanza.Nikama walishajiandaa kwa ajali maana baadhi yao walipotujia walikuwa na mitungi ya oksijeni migongoni”,akina mama hao walisema.
Baadhi yao waliniambia,ingekuwa heri kama serikali ingefanya uchunguzi kuhusu ajali ile hivi sasa,kuona kama kulikuwa na kitu kilichofichwa.
Hata hivyo,serikali ilisisitiza kuwa ajali ile haikuwa hujuma ya wafanyakazi wa TRC ambao baada ya treni kurudi nyuma na kuacha njia,walitokomea.
Abiria wengi walikufa kwa kukosa hewa,baada ya mabehewa kugongana na kupandana,vumbi na moshi vikajaa ndani ya mabehewa.
Nawakumbuka baadhi ya Marehemu:Agnes Thomas(Shinyanga),Revoca Mkama,Prisca Hunzebe ambaye alikuwa mtoto wa miaka minne,hawa walitoka Jijini Mwanza.
Wengine waliokufa ni Leah Isaka,Ayoub Isaka, Mariam Mgumba,Hapines Kaswamira,Jackline Kasika,Roda Kasika na Nyangeta Kasika hawa wa familia moja,waliozikwa Suguti,Majita Musoma.
Hakika,walikuwa wengi na orodha ni ndefu.
Miongoni mwa walionusurika ni Bibi Elizabeth Mkungu ambaye ni Mshiriki wa Kanisa la Kirumba,ambaye  hata sasa ni mwimbaji mwaminifu wa  kwaya ya Kirumba Adventist Women Ministry(AWM).
Amewahi kutoa ushuhuda katika wimbo unaoimbwa na kwaya ya Kirumba Adventist(KAC) huku akibubujikwa machozi.Aliumia vibaya na kulazimika kufanyiwa Operesheni kadhaa.
Wakati huo,Mkurugenzi Mkuu wa TRC alikuwa Liniford Mboma,alikuwa nyuma ya Waziri Mkuu kupinga mawazo kwamba wafanyakazi wa TRC waliihujumu treni ile.
Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,Prof.Mark James Mwandosya,naye alisema hakukuwa na ukweli kwamba wafanyakazi wa TRC wangejitoa mhanga na kufa katika ajali ile.
Hata hivyo,ilisemwa walikuwa na ‘mitungi ya oksijeni’ migongoni.Wakati treni ile ikirudi kinyume-nyume,tena kwa kasi ya kutisha,hakuna aliyejua kilichotokea, yawezekana waliruka na kunusurika.
Mbunge wa Busega wakati huo,Raphael Masunga Chegeni alisema katika Jimbo lake,watu takriban walipoteza maisha,miongoni mwao akina mama hao wa Women Ministry.Hata Jimbo la Nyang’wale walikuwepo akina mama hao wakitoka Morogoro.
    KWAYA YA PATMOS
Ajali ile iliwakumba baadhi ya waimbaji wa Kwaya ya Patmos kutoka mjini Shinyanga,baadhi yao walifariki na wengine kunusurika baadhi ya kujeruhiwa vibaya.
Kirumba,walipoteza walishiriki wengi,baadhi yao ni Prisca Mwijarubi,na wengine walitoka Pasiansi ambao ni Wittiness Pares,Restituta John na Rose Fidel.
Watu watatu wa familia moja walipoteza uhai katika janga lile,mmoja akanusurika ambaye ni Swamila Kasika.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI

SABATO YA TAREHE 6/6/2015. Muziki wa Kikristo, kichocheo cha afya na tiba.

Na Conges Mramba,Kirumba


SEMINA ya Muziki iliyoanza  Jumatano,Juni 3 imetia nanga Katika Kanisa
la  Waadventista wa Sabato Kirumba Jijini Mwanza  Sabato ya Juni
6,huku Jamii nzima ya waimbaji nchini Tanzania ikitakiwa kumtukuza
Mungu kwa kuimba nyimbo zenye kuzingatia Kanuni, Biblia na Roho ya
Unabii.
Mkufunzi wa semina hiyo,Dk.Samweli Tumaini Mugaya(PhD), ambaye ni
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, amesema aghalabu nyimbo huimbwa nje
ya taaluma na kanuni mahsusi za uimbaji,
Akitoa mfano,amesema waimbaji huimba pasipokufuata mapigo ya
nyimbo,hali inayosababishwa nyimbo kuimbwa vibaya hata pasipo
kuzingatia tune husika za nyimbo nyakati za ibada.
Dk.Samweli Mgaya amesisitiza uimbaji bora unaozingatia maadili ya
taaluma ya muziki ili kufariji washiriki na kuinua myoyo yao kwa
Kristo nyakati za Ibada.
“SAUTI NYINGI,WIMBO MMOJA”ndiyo kauli mbiu iliyotumika wakati wa
mafunzo hayo ya taaluma ya kuziki katika Kanisa la Waadventista wa
Sabato,ambayo yaliwahusisha washiriki wa makanisa ya Jijini Mwanza.
Hata hivyo,Dk. Mugaya amesema uimbaji una faida mbalimbali kiafya,kwa
kuwa huondoa msongo wa mawazo(Stress),huimarisha kinga ya
mwili,huwafanya waimbaji kukumbuka mafundisho ya kiroho,wakati pia
nyimbo hufariji na ni maombi halisi kwa Mungu.
Kulingana na TAFSIRI ya Shirika la Afya la Umoja wa
Mataifa(WHO)iliyotolewa mwaka 1948,Afya ni Ukamilifu wa
Kimwili,Kiroho,Kiakili na Mahusiano ya kufaa na Jamii nzima.
“Kwa sababu zilizotajwa na WHO,uimbaji huwafanya waimbaji kuwa na
mahusiano mazuri,kwa kuwa hukaa muda mrefu wakiimba pamoja na
kudumisha udugu na upendo”,Dk.Mugaya amesisistiza.
Akawashauri waimbaji kuzingatia mazoezi ya mwili na kanuni ya chakula
bora,unywaji wa maji salama  ya kutosha,huku wakiepuka vyakula vya
chumvi nyingi  na soda.
“Mboga za majani,matunda na viungo kama vitunguu saumu ni muhimu kwa
watu wanaojikuta sauti zikikwama”,amesema.
Akichangia,Mwalimu wa Kwaya ya Kirumba,Dk.Darlington Onditi,amesema
jamii ya vinywaji aina ya soda kwa waimbaji,huwasababishia sauti
kukwama.
Waimbaji pia wameshauriwa kutokukaa kwenye viyoyozi muda mrefu,kwa
kuwa  mapangaboi na viyoyozi huwa na tabia ya kukausha sauti pindi
wanapoimba.
“Tujitahidi kutumia hewa safi ambayo Mungu ameiumba,badala ya kutumia
hewa zisizoasili;ambazo huathiri afya hususan kwa waimbaji”,Dk.Mugaya
amesisitiza.

HUDUMA YA UTANDAAJI KATIKA KITUO CHA WATOTO WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU YAFANA.

Na Kamati ya Mawasiliano Kirumba.
Mnamo tarehe 30/05/2015 Jumamosi siku ya Sabato, Watoto wa kanisa la Waadventista Wasabato Kirumba walifanya huduma ya utandaaji katika kituo cha watoto waishio katika mazingira magumu wanaolelewa na kituo cha Foundation Karibu Tanzania. 
Watoto walishirikiana kuimba pamoja, mafundisho ya neno la Mungu yalitolewa. na Mkuu wa Idara ya Watoto kanisa la Kirumba mama Debora Ngissa akishirikiana na walimu wa watoto wa kanisa hilo Bi Betty Njile na Bi Eza Kabuche walikuwa wawezeshaji wa tukio hilo makini.
Aidha kanisa la Waadventista Wasabato Kirumba kupitia idara ya watoto ilitoa zawadi ya dawa ya kutibu vidonda na pesa tasilimu ya kununulia chakula kwaajili ya watoto wa kituo hicho. Kwa ujumla watoto na walezi wa kituo hicho cha Foundation Karibu Tanzania wamefarijika sana na kutoa shukrani zao za dhati kwa kanisa la Kirumba kupitia Idara ya watoto kwa jinsi inavyojali na kuonesha kwa vitendo Upendo wa Mwenyezi Mungu.

   MATUKIO ZAIDI KATIKA PICHA









Hospitali ya Pasiansi mbioni kukamilika

Na Kamati ya Mawasiliano,Kirumba

HOSPITALI ya Waadventista wa Sabato, Mwanza Adventist Medical Centre(MAMC),sasa iko katika hatua za mwisho za Ujenzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idaraya Afya ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania (NTUC), Dk Silas Kabhele, amesema zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu zimetumika kujenga Hospitali hiyo.

Hospitali ya Pasiansi inavoonekana sasa
                                          
 Dk.Kabhele ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Afya katika Jimbo  la Kusinim wa Ziwa Nyanza(SNC) amesema Siku ya Sabato Mei 30 kwamba sasa zinahitajika takriban shilingi milioni 600 kukamilisha ujenzi.
Akizungumza wakati wa Huduma Kuu katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Kirumba Jijini Mwanza,Dk.Kabhele amesema Hospitali hiyo ya Gorofa tano tayari paa limeezekwa,kuta zote za nje zimepigwa lipu; na kwamba hata baadhi ya kuta za ndani zimepigwa lipu.
“Takriban shilingi bilioni 1.6 zimekusanywa kutoka kwetu na kutoka kwa rafiki zetu; kazi zilizobaki ni kumalizia lipu ndani, kuweka sakafu, madirisha, milango, kupakarangi, kuingiza umeme na maji na kusimika mitambo ya usalama”,Dk. Kabhele amebainisha.
Jengo la Hospitali ya Pasiansi limefikia hapa
 Aidha, amesisitiza kuwa Hospitali itakapoanza kazi, itakuwa kituo cha  Uinjilisti, ambayo ndiyo njia ya pekee ya kuisaidia jamii isiyomjua Mungu kuja wenyewe kwaYesu Kristo.
“Wale ,hujakutafuta huduma ya Afya; na hivyo hupata Injili itakayokuwa ikitolewa sambamba na huduma zetu za afya”,Dk. Kabhele amesisitiza. 

Akasema, "sasa Zinahitajika shilingi milioni 600 kukamilisha kazi hiyo ya Ujenzi wa Hospitali hiyo".
Jiwe la Msingi la Hospitali hiyo liliwekwa na Rais Jakaya Kikwete Septemba 8 mwaka 2013; na Hospitali hiyo ilitazamiwa kufunguliwa rasmi mwaka huu wakati wowote ikikamilika.
Akizungumzia vifaavya tiba,Mkurugenzi huyo wa Afyaamesema, tayari Kontena mbili za vifaa vimekwisha tumwa kutoka Uswisi, na Wajerumani wameahidi kuleta vingine kwa ajili ya kuanza kazi baada ya ujenzi kukamilika.
Kulingana na Kamati ya Ujenzi, kila Mtaa katika Jimbo la SNC umepangiwa goli lake.

 Hospitali hiyo itakapokamilika, itakuwa na vyuo mbalimbali vya Sayansi ya Tiba, na itakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa wagonjwa 200 kila siku, pia itakuwa na jumla ya vitanda 450  vya kulaza wagonjwa.
Hospitali ya Pasiansi ikikamilika itafanana hivi
Aidha,Dk.Kabhele 
amewomba wadau wote wa Huduma za Jamii kuchangia mradi huu toka kona zote za nchi kuingiza michango yao katika akaunti ya ujenzi wa hospitali hii:
Jina la akaunti: Pasiansi SDA Hospital Fund,
Akauntinamba:      01J1060067500
Benki: CRDB


LESONI JUMAPILI:MAMLAKA YA YESU KRISTO BWANA WETU

SOMO KWA UFUPI
Kama tabibu na Msomi mkubwa Luka alikuwa na mamlaka makubwa sana.Alikuwa na Uelewa mkubwa sana katika falsafa za Kigiriki kwa wakati ule, kwa sababu alikuwa amesoma sana.Alifahamu pia mamlaka ya sheria za kirumi katika maswala ya kijamii na serikali yao kwa ujumla.Akiwa kama msafiri mwenza wa Paulo,Na walikuwa na mamlaka makubwa sana katika makanisa waliyokuwa wakiyatembelea.

MASWALI NA MAFUNGU MUHIMU YA KUJIULIZA:
SOMA : Luka 8:22-25Luka 4:31-37Luka 5:24-26Luka 7:49Luka12:8. Ni aina gani ya madaraka yesu alikuwa nayo na ambayo alifanya kazi kwayo?

Binadamu wengi sana wanafanya mambo mengi katika jina la Mungu,kitu ambacho kwa kiasi kikubwa huwapa mamlaka makubwa katika matendo yao.Tunawezaje kufahamu au kutambua kuwa tunaposema,"Mungu naomba nifanye hili" Tunawezaje kutambua kuwa ameturuhusu kufanya jambo hilo??

SABATO YA TAREHE 23/5/2015 Wasabato watakiwa kurejea tabia ya Kanisa la Mitume


"Nawaambia hivi, Kuomba kwa nia ya kufanya matengenezo ni lazima....",Mchungaji Beatus Mlozi
Yasisitizwa, bila kufanana na Mitume,hakuna atakayemwona Mungu!
Na Conges Mramba,Mwanza
MKURUGENZI wa Idara ya Uchapaji katika Jimbo la Kusini mwa Ziwa Nyanza(SNC),Beatus Mlozi,amesema Washiriki wa Kanisa la Waadventista wa Sabato wanapaswa kufanya Matengenezo na kurejea tabia zilizokuwemo katika Kanisa la Mitume.
Mchungaji Mlozi amesema Kanisa la Mitume liliongezeka idadi ya washiriki wake na viwango vya Ubora wa kiroho,kwa njia ya Kujifunza pamoja Neno la Mungu,Kushiriki Meza ya Bwana,kupendana wao kwa wao na kudumu katika maombi.
Akihutubu Huduma Kuu katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Kirumba,Jijini Mwanza Sabato mchana,Mei 23,Mchungaji Mlozi amemtaka kila mshiriki wa Kanisa kufanya Matengenezo, ili kufanana na Kanisa la Kwanza la Mitume.
“Ni jambo muhimu kwa kuwa hakuna atakayeingia Mbinguni asipokuwa na Utakatifu uliokuwemo miongoni wa washiriki wa Kanisa la kwanza la Mitume.”,amesema Mch.Mlozi.
Kauli ya Mkurugenzi huyo wa Idara ya Uchapaji ya South Nyanza Conference, imekuja kukiwa na changamoto ya washiriki wapya kutodumu katika Ushirika,kufuatia hali ya washiriki wa zamani kupooza na kutokuwa na viwango vya Ubora kama vinavyoainishwa katika tabia za Kanisa hilo la Mitume.
“Kama kanisa linakua,nawe mshiriki hukui, maana yake hauko kwenye kanisa lile.”amesisitiza.
Kanisa la Mitume lilikua kwa njia ya waumini wake kuongezeka kufuatia kusikia Injili.
“Kanisa linakua kwa njia ya Kuhubiri Injili,kanisa linalokua ni lile linalohubiri Habari Njema ya Wokovu”,amefafanua.
Alisema, washiriki wa Kanisa la Mitume walidumu kanisani wakimega mkate;wakishiriki chakula chao kwa furaha, wakiwapendeza watu wote.
Akaonya kwamba leo Washiriki wameshindwa kula chakula pamoja,na kwa sababu kanisa limepoteza ushirikiano, Kanisa limepoteza hata tabia zilizokuwemo miongoni mwa washiriki wa Kanisa la zama za Mitume(1-100 `AD).
Alifafanua kuwa Kanisa la Mitume walizingatia vitu vitano:
• Walidumu katika Chumba cha Juu(Upper Chamber) wakiomba na kungoja ahadi ya Roho Mtakatifu.Wenye chuki na magomvi miongoni mwao hawakudumu katika chumba hicho cha Juu. Walitunza mahusiano ndani ya Kanisa
• Waliodumu chumba cha Juu wakingoja Roho Mtakatifu,walisameheana,wakatengeneza Umoja(Matengenezo)halisi ya kiroho-Spiritual Reformation, ni muhimu katika Ujenzi wa Kanisa leo.
Walidumu kusubiri Roho Mtakatifu,Walidumu katika Mafundisho ya Mitume,ni kujifunza neno la Mungu kwaa bidii nyingi.
• Walidumu katika Ushirika(Fellowship);ni udugu(Brotherhood);kutembeleana,kusaidiana na kubebeana mizigo.Kanisa la Mitume halikuruhusu familia moja miongoni mwao kulala njaa.
• Kuumega Mkate(Lord’s Supper) na Chakula cha kawaida wanachosaidiana washiriki wanapokula pamoja.Familia zilikuwa na tabia ya kula pamoja chakula,kwa sababu hiyo, upendo wa kidugu(Brotherhood)ulidumu miongoni mwao.
• Maombi huongeza ubora wa ubora wa kiroho,na kumfanya Mshiriki wa Kanisa kuzungumza na Mungu;ni kukiendea Kiti cha Rehema.
“Hiyo tabia ya kula chakula pamoja imekwenda wapi? Hata tabia ya kula makande pamoja imekwenda wapi?”Pr.Mlozi akahoji.
Kufuatia hali hiyo, washiriki walishikamana. “Mshiriki anayekuja kukutembelea,amechukua sehemu ya maisha yake kukuthamini”,amesema.
Akasisitiza kwamba washiriki wametakiwa kurejea tabia ya Kanisa la Mitume kwa kutenda haya na kuutafuta Utakatifu ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao.

church Choir


 

Copyright ©2015 KIRUMBA ADVENTIST CHURCH