KUMBUKUMBU YA MIAKA 13 YA AJALI YA TRENI, DODOMA.

Ulikuwa Msiba mkubwa wa Waadventista wa Sabato Tanzania
Na Conges Mramba,Mwanza
JUMATANO,Juni 24 mwaka huu 2015, itatimia miaka 13 tangu ilipotokea ajali ya Treni,huko Igandu na Msagali Mkoani Dodoma na kuua takriban watu 400, huku zaidi ya 700 wakinusurika.
Kumbukumbu hii inatonesha donda katika myoyo ya Washiriki wa Makanisa ya Waadventista wa Sabato hususan wa Mikoa yote ya Ukanda wa Ziwa,likiwemo kanisa la Kirumba.
Ajali hii ya Kihistoria,mbali na kuua Watanzania wengi,ni Kumbukumbu ya Kihistoria kwa Kanisa la Waadventista wa Sabato hapa nchini Tanzania,na dunia nzima.
Wakati huo,hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan,alituma rambirambi.
Hata Papa John Paul,Kiongozi wa Kanisa Katoliki,alituma salamu za pole kwa Watanzania.Hukuwa msiba wetu peke yetu.
Zaidi ya wanawake 120 waumini wa Kanisa hili waliteketea katika ajali hiyo ya Alhamisi,Juni 24 mwaka 2002,iliyotokea Asubuhi hiyo eneo hilo kati ya Igandu na Msagali.

Hawa wengi walikuwa akina mama wa mikoa ya Mwanza,Shinyanga,Mara na Kigoma,waliokuwa wakitokea mjini Morogoro.
Juni 18 hadi Juni 22 mwaka huo 2002 kulikuwa na Mkutano wa akina mama Waadventista wa Sabato(Adventist Women Ministry Congress) hapo mjini Morogoro.
Akina mama wa Kanisa hili kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu walikwenda kuhudhuria Mkutano ule.Mkutano ule ulihitimishwa siku ya Sabato,Juni 22. Walikuwa zaidi ya 400.
Ilipofika Jumapili,Juni 23 walikwea treni tayari kurejea nyumbani,baada ya Mkutano ule kumalizika.
Wengi walipanda mabehewa ya Daraja la tatu ambayo yalikuwa na nambari 362211,364P,3635,3620M,3642,3617 na 3680.
Mabehewa hayo yalibeba wanafunzi na akina mama hao wa Ki-Sabato.
Nakumbuka,wakati huo nikifanya kazi katika Gazeti la Msanii Afrika, lililomilikiwa na Kampuni ya Sahara Media Group ambayo sasa inamiliki kituo cha Televisheni cha Star,Kiss FM,Radio Free Afrika na King’amuzi cha Continental, nilitumwa kufuatilia ajali ile katika Makao Makuu ya Jimbo la Kusini mwa Ziwa Nyanza(SNC),Pasiansi.
Nilimkuta Mchungaji  Daudi Makoye(Sasa Mwenyekiti wa Mara Conference),ambaye hakuwa tayari kutoa tamko.Hata wafanyakazi wengine hapo Pasiansi,hawakuwa tayari kusema kitu,wakati Mwenyekiti wa SNC niliambiwa alikuwa kaondoka siku hiyo kwenda Dodoma kutambua maiti.
Mwanamke mmoja,aliniambia kwa masharti ya kutotajwa jina kwamba wanawake takriban 100 wa makanisa ya Mwanza tu waliangamia katika ajali ile ya kutisha.
“Jana Alasiri(Juni 24) tulipata simu kutoka Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma,kwamba kati ya maiti 200 waliokuwepo uwanjani hapo;100 ni Wasabato wa mikoa ya Mwanza,Mara,Shinyanga na Kigoma!”Ofisa huyo wa Jimbo la South Nyanza aliniambia.
Nilikwenda Ofisini(Ilemela)nikaandika habari iliyotoka kwa kichwa cha habari, “Waumini 100 wa  Kanisa la Wasabato wahofiwa kufa!”
Nilifika Kanisa la Mabatini mchana,nikakuta watu wakilia,niliambiwa Kirumba na Pasiansi kulikuwa na kilio kikubwa…Bunda,Musoma,Tarime,Busega na hata vijiji vya Suguti huko Majita Mkoani Mara kulikuwa na majonzi makubwa.Ulikuwa msiba mkubwa,msiba wa kila mtu.
Naam, miaka 13 imepita sasa tangu ajali ile ya kutisha itokee.Wengi wamesahau,ndiyo maana tunawakumbusha hapa.
  
         ILIKUWA AJALI YA KUPANGWA?
Waziri mkuu,Frederick Tluway Sumaye(wakati huo),alisema ajali ile iliyotokea Dodoma na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 250 haikuwa hujuma,bali ajali ya kawaida ya kibinadamu(Tragic accident).
Wakati huo,kulikuwa na mgogoro baina ya wafanyakazi na Menejimenti ya lililokuwa Shirika la Reli(TRC),wakidai mafao yao.
Miaka micache baadaye,nilihudhuria msiba wa mmoja wa wafanyakazi wa SOUTH NYANZA CONFERENCE nikawasikia baadhi ya akina mama walionusurika katika ajali ile wakisema,ilikuwa ajali ya kupangwa.
“Walitusimanga(wafanyakazi wa treni ile),walikuwa wakitwambia tungeona hata kabla ya safari kuanza.Nikama walishajiandaa kwa ajali maana baadhi yao walipotujia walikuwa na mitungi ya oksijeni migongoni”,akina mama hao walisema.
Baadhi yao waliniambia,ingekuwa heri kama serikali ingefanya uchunguzi kuhusu ajali ile hivi sasa,kuona kama kulikuwa na kitu kilichofichwa.
Hata hivyo,serikali ilisisitiza kuwa ajali ile haikuwa hujuma ya wafanyakazi wa TRC ambao baada ya treni kurudi nyuma na kuacha njia,walitokomea.
Abiria wengi walikufa kwa kukosa hewa,baada ya mabehewa kugongana na kupandana,vumbi na moshi vikajaa ndani ya mabehewa.
Nawakumbuka baadhi ya Marehemu:Agnes Thomas(Shinyanga),Revoca Mkama,Prisca Hunzebe ambaye alikuwa mtoto wa miaka minne,hawa walitoka Jijini Mwanza.
Wengine waliokufa ni Leah Isaka,Ayoub Isaka, Mariam Mgumba,Hapines Kaswamira,Jackline Kasika,Roda Kasika na Nyangeta Kasika hawa wa familia moja,waliozikwa Suguti,Majita Musoma.
Hakika,walikuwa wengi na orodha ni ndefu.
Miongoni mwa walionusurika ni Bibi Elizabeth Mkungu ambaye ni Mshiriki wa Kanisa la Kirumba,ambaye  hata sasa ni mwimbaji mwaminifu wa  kwaya ya Kirumba Adventist Women Ministry(AWM).
Amewahi kutoa ushuhuda katika wimbo unaoimbwa na kwaya ya Kirumba Adventist(KAC) huku akibubujikwa machozi.Aliumia vibaya na kulazimika kufanyiwa Operesheni kadhaa.
Wakati huo,Mkurugenzi Mkuu wa TRC alikuwa Liniford Mboma,alikuwa nyuma ya Waziri Mkuu kupinga mawazo kwamba wafanyakazi wa TRC waliihujumu treni ile.
Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,Prof.Mark James Mwandosya,naye alisema hakukuwa na ukweli kwamba wafanyakazi wa TRC wangejitoa mhanga na kufa katika ajali ile.
Hata hivyo,ilisemwa walikuwa na ‘mitungi ya oksijeni’ migongoni.Wakati treni ile ikirudi kinyume-nyume,tena kwa kasi ya kutisha,hakuna aliyejua kilichotokea, yawezekana waliruka na kunusurika.
Mbunge wa Busega wakati huo,Raphael Masunga Chegeni alisema katika Jimbo lake,watu takriban walipoteza maisha,miongoni mwao akina mama hao wa Women Ministry.Hata Jimbo la Nyang’wale walikuwepo akina mama hao wakitoka Morogoro.
    KWAYA YA PATMOS
Ajali ile iliwakumba baadhi ya waimbaji wa Kwaya ya Patmos kutoka mjini Shinyanga,baadhi yao walifariki na wengine kunusurika baadhi ya kujeruhiwa vibaya.
Kirumba,walipoteza walishiriki wengi,baadhi yao ni Prisca Mwijarubi,na wengine walitoka Pasiansi ambao ni Wittiness Pares,Restituta John na Rose Fidel.
Watu watatu wa familia moja walipoteza uhai katika janga lile,mmoja akanusurika ambaye ni Swamila Kasika.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI

Tupe maoni yako hapo chini..!

Share this article :

'LIKE' UKURASA WETU WA FACEBOOK HAPO CHINI...!

0 comments:

Post a Comment

 

Copyright ©2015 KIRUMBA ADVENTIST CHURCH